35. Faatir - Qurani
- 1. Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi, aliye wafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa, mbili-mbili, na tatu- tatu, na nne-nne. Huzidisha katika kuumba apendavyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.
- 2. Rehema ambayo Mwenyezi Mungu anawafungulia watu hapana wa kuizuia. Na anayo izuia hapana wa kuipeleka isipo kuwa Yeye. Naye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
- 3. Enyi watu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu. Ati yupo muumba mwengine asiye kuwa Mwenyezi Mungu anaye kupeni riziki kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Hapana mungu ila Yeye tu. Basi wapi mnako geuzwa?
- 4. Na wakikukanusha, basi walikwisha kanushwa Mitume kabla yako. Na mambo yote yatarudishwa kwa Mwenyezi Mungu.
- 5. Enyi watu! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala mdanganyifu asikudanganyeni juu ya Mwenyezi Mungu.
- 6. Hakika Shet`ani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa ni adui. Kwani yeye analiita kundi lake liwe katika watu wa Motoni.
- 7. Walio kufuru watakuwa na adhabu kali; na walio amini na wakatenda mema watapata msamaha na ujira mkubwa.