• 1. Naapa kwa pepo zinazo tawanya,

  • 2. Na zinazo beba mizigo,

  • 3. Na zinazo kwenda kwa wepesi.

  • 4. Na zinazo gawanya kwa amri,

  • 5. Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka ni kweli,

  • 6. Na kwa hakika malipo bila ya shaka yatatokea.

  • 7. Naapa kwa mbingu zenye njia,

  • 8. Hakika nyinyi bila ya shaka mmo katika kauli inayo khitalifiana.

  • 9. Anageuzwa kutokana na haki mwenye kugeuzwa.

  • 10. Wazushi wameangamizwa.

  • 11. Ambao wameghafilika katika ujinga.

  • 12. Wanauliza: Ni lini hiyo siku ya malipo?

  • 13. Hiyo ni siku watakayo adhibiwa Motoni.

  • 14. Onjeni adhabu yenu! Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyahimiza.

  • 15. Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem.

  • 16. Wanapokea aliyo wapa Mola wao Mlezi. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema.

  • 17. Walikuwa wakilala kidogo tu usiku.

  • 18. Na kabla ya alfajiri wakiomba maghfira.

  • 19. Na katika mali yao ipo haki ya mwenye kuomba na asiye omba.

  • 20. Na katika ardhi zipo Ishara kwa wenye yakini.

  • 21. Na pia katika nafsi zenu - Je! Hamwoni?

  • 22. Na katika mbingu ziko riziki zenu na mliyo ahidiwa.

  • 23. Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, hakika haya ni kweli kama ilivyo kweli kuwa nyinyi mnasema.

  • 24. Je! Imekufikia hadithi ya wageni wa Ibrahim wanao hishimiwa?

  • 25. Walipo ingia kwake wakasema: Salama! Na yeye akasema: Salama! Nyinyi ni watu nisio kujueni.

  • 26. Akenda kwa ahali yake na akaja na ndama aliye nona.

  • 27. Akawakaribisha, akasema: Mbona hamli?

  • 28. Akahisi kuwaogopa katika nafsi yake. Wakasema: Usiwe na khofu, nao wakambashiria kupata kijana mwenye ilimu.

  • 29. Ndipo mkewe akawaelekea, na huku anasema na akijipiga usoni kwa mastaajabu, na kusema: Mimi ni kikongwe na tasa!

  • 30. Wakasema: Ndivyo vivyo hivyo alivyo sema Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mwenye kujua.

  • 31. AKASEMA: Basi ujumbe wenu ni nini, enyi mlio tumwa?

  • 32. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa watu wakosefu,

  • 33. Tuwatupie mawe ya udongo,

  • 34. Yaliyo tiwa alama kutoka kwa Mola wako Mlezi kwa ajili ya wanao pindukia mipaka.

  • 35. Kwa hivyo tutawatoa katika hao wale walio amini.

  • 36. Lakini hatukupata humo ila nyumba moja tu yenye Waislamu!

  • 37. Na tukaacha humo Ishara kwa ajili ya wanao iogopa adhabu chungu.

  • 38. Na katika khabari za Musa, tulipo mtuma kwa Firauni na hoja wazi.

  • 39. Lakini alipuuza kwa sababu ya nguvu zake na akasema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu!

  • 40. Basi tukamkamata yeye na majeshi yake na tukawatupa baharini, na yeye ndiye wa kulaumiwa.

  • 41. Na katika khabari za A`di tulipo wapelekea upepo wa kukata uzazi.

  • 42. Haukuacha chochote ulicho kifikia ila ulikifanya kama kilio nyambuka.

  • 43. Na katika khabari za Thamudi walipo ambiwa: Jifurahisheni kwa muda mdogo tu.

  • 44. Wakaasi amri ya Mola wao Mlezi. Basi uliwanyakua moto wa radi nao wanaona.

  • 45. Basi hawakuweza kusimama wala hawakuwa wenye kujitetea.

  • 46. Na kaumu ya Nuhu hapo mbele. Hakika hao walikuwa watu wapotovu.

  • 47. Na mbingu tumezifanya kwa nguvu na uwezo na hakika Sisi bila ya shaka ndio twenye uwezo wa kuzitanua.

  • 48. Na ardhi tumeitandaza; basi watandazaji wazuri namna gani Sisi!

  • 49. Na katika kila kitu tumeumba kwa jozi ili mzingatie.

  • 50. Basi kimbilieni kwa Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake.

  • 51. Wala msifanye kuwa kuna mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake.

  • 52. Basi ndio hivyo hivyo, hakuwajia kabla yao Mtume ila walisema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu.

  • 53. Je! Wameambizana kwa haya? Bali hawa ni watu waasi.

  • 54. Basi waachilie mbali, nawe hulaumiwi.

  • 55. Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa Waumini.

  • 56. Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.

  • 57. Na sitaki kwao riziki, wala sitaki wanilishe.

  • 58. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti.

  • 59. Hakika walio dhulumu wana fungu lao la adhabu kama fungu la wenzao. Basi wasinihimize.

  • 60. Ole wao walio ikanusha siku yao waliyo ahidiwa.