• 1. Alif Lam Ra. (A. L. R). Hizi ni Aya za Kitabu na Qur`ani inayo bainisha.

  • 2. HUENDA ikawa walio kufuru wakatamani wange kuwa Waislamu.

  • 3. Waache wale, na wastarehe, na iwazuge tamaa. Watakuja jua.

  • 4. Na hatukuuangamiza mji wowote ule ila ulikuwa na muda wake maalumu.

  • 5. Hawawezi watu wowote kuitangulia ajali yao, wala kuchelewa.

  • 6. Na walisema: Ewe uliyeteremshiwa Ukumbusho! Hakika wewe ni mwendawazimu.

  • 7. Mbona hutuletei Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli?

  • 8. Sisi hatuwateremshi Malaika ila kwa sababu ya haki, na hapo hawatapewa muhula.

  • 9. Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutao ulinda.

  • 10. Na hakika tulikwisha watumia Mitume mataifa ya mwanzo.

  • 11. Na hakuwafikia Mtume ila walimkejeli.

  • 12. Na kama hivi ndivyo tunavyo ingiza katika nyoyo za wakosefu.

  • 13. Hawayaamini haya, na hali ya kuwa umekwisha wapitia mfano wa watu wa kale.

  • 14. Na lau tungeli wafungulia mlango wa mbingu, wakawa wanapanda,

  • 15. Basi wangeli sema: Macho yetu yamelevywa, bali sisi wenyewe tumerogwa.

  • 16. Na hakika tumeweka katika mbingu vituo vya sayari, na tumezipamba kwa wenye kuangalia.

  • 17. Na tumezilinda na kila shetani afukuzwaye.

  • 18. Isipo kuwa mwenye kusikiliza kwa kuibia, naye hufuatwa na kijinga cha moto kinacho onekana.

  • 19. Na ardhi tumeitandaza na humo tumeweka milima, na tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake.

  • 20. Na tumekujaalieni humo vitu vya maisha yenu, na ya hao ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku.

  • 21. Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na Sisi; wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu.

  • 22. Na tunazipeleka pepo za kupandishia, na tunateremsha kutoka mbinguni maji, kisha tukakunywesheni maji hayo. Wala si nyinyi mnayo yaweka.

  • 23. Na Sisi ndio tunao huisha na tunao fisha. Na Sisi ndio Warithi.

  • 24. Na tunawajua walio tangulia katika nyinyi, na tunawajua walio taakhari.

  • 25. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye atakaye wakusanya. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mjuzi.

  • 26. Na tulimuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura.

  • 27. Na majini tuliwaumba kabla kwa moto wa upepo umoto.

  • 28. Na Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Hakika Mimi nitamuumba mtu kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yaliyo tiwa sura.

  • 29. Basi nitakapo mkamilisha na nikampulizia roho yangu, basi mumwangukie kumsujudia.

  • 30. Basi Malaika wote pamoja walimsujudia,

  • 31. Isipo kuwa Iblisi. Yeye alikataa kuwa pamoja na walio sujudu.

  • 32. (Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na walio sujudu?

  • 33. Akasema: Haiwi mimi nimsujudie mtu uliye muumba kwa udongo unao toa sauti, unao tokana na matope yenye sura.

  • 34. (Mwenyezi Mungu) akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe ni maluuni!

  • 35. Na hakika juu yako ipo laana mpaka Siku ya Malipo.

  • 36. Akasema (Iblisi): Mola wangu Mlezi! Nipe muhula mpaka siku watapo fufuliwa.

  • 37. (Mwenyezi Mungu) akasema: Hakika wewe ni katika walio pewa muhula

  • 38. Mpaka siku ya wakati maalumu.

  • 39. Akasema: Mola wangu Mlezi! Ilivyo kuwa umenitia makosani, basi nahakikisha nitawazaini hapa duniani na nitawapoteza wote,

  • 40. Ila waja wako walio safika.

  • 41. Akasema: Hii Njia ya kujia kwangu Iliyo Nyooka.

  • 42. Hakika waja wangu, wewe hutakuwa na mamlaka juu yao, isipo kuwa wale wapotofu walio kufuata.

  • 43. Na bila shaka Jahannamu ndipo pahali pao walipo ahidiwa wote.

  • 44. Ina milango saba; na kwa kila mlango iko sehemu walio tengewa.

  • 45. Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem.

  • 46. (Wataambiwa:) Ingieni kwa salama na amani.

  • 47. Na tutaondoa chuki iliyo kuwamo vifuani mwao, wawe ndugu juu ya viti vya enzi wameelekeana.

  • 48. Humo hayatawagusa machofu, wala hawatatolewa humo.

  • 49. Waambie waja wangu ya kwamba Mimi ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

  • 50. Na kwamba adhabu yangu ndio adhabu iliyo chungu!

  • 51. Na uwape khabari za wageni wa Ibrahim.

  • 52. Walipo ingia kwake na wakasema: Salama! Yeye akasema: Hakika sisi tunakuogopeni.

  • 53. Wakasema: Usiogope. Sisi tunakubashiria kijana mwenye ujuzi.

  • 54. Akasema: Mnanibashiria nami uzee umenishika! Basi kwa njia gani mnanibashiria?

  • 55. Wakasema: Tunakubashiria kwa haki; basi usiwe miongoni mwa wanao kata tamaa.

  • 56. Akasema: Na nani anaye kata tamaa na rehema ya Mola wake Mlezi ila wale walio potea?

  • 57. Akasema: Hebu nini amri yenu, enyi wajumbe?

  • 58. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wakosefu!

  • 59. Isipo kuwa walio mfuata Luut`i. Bila ya shaka sisi tutawaokoa hao wote.

  • 60. Ila mkewe. Tunakadiria huyo atakuwa miongoni watao bakia nyuma.

  • 61. Basi wale wajumbe walipo fika kwa Luut`i,

  • 62. Alisema (Luut`i): Hakika nyinyi ni watu msio juulikana.

  • 63. Wakasema: Bali sisi tumekuletea yale waliyo kuwa wakiyafanyia shaka.

  • 64. Na tumefika kwako kwa Haki, na hakika sisi tunasema kweli.

  • 65. Basi ondoka na ahli zako usiku ungalipo, nawe ufuate nyuma yao, wala yeyote kati yenu asigeuke nyuma. Na mwende mnapo amrishwa.

  • 66. Na tukamfunulia hukumu hiyo, ya kwamba hata wa mwisho wao hao ikifika asubuhi atakuwa kesha katiliwa mbali.

  • 67. Na wakaja watu wa mji ule nao furahani.

  • 68. Akasema: Hakika hawa wageni wangu, basi msinifedheheshe.

  • 69. Na mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi.

  • 70. Wakasema: Sisi hatukukukataza usimkaribishe yeyote?

  • 71. Akasema: Hawa binti zangu, ikiwa nyinyi ni watendaji.

  • 72. Naapa kwa umri wako! Hakika hao walikuwa katika ulevi wao, wakihangaika ovyo.

  • 73. Ukelele ukawatwaa wakipambaukiwa.

  • 74. Na tukaigeuza nchi juu chini, na tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo wa Motoni.

  • 75. Hakika katika hayo zipo ishara kwa waaguzi.

  • 76. Na miji hii ipo kwenye njia inayo pitiwa.

  • 77. Hakika katika hayo ipo ishara kwa Waumini.

  • 78. Na hakika watu wa Kichakani walikuwa wenye kudhulumu.

  • 79. Kwa hivyo tukawaadhibu. Na nchi mbili hizi ziko kwenye njia ilio wazi.

  • 80. Na bila ya shaka wakaazi wa Hijr waliwakanusha Mitume.

  • 81. Na tuliwapa ishara zetu, nao wakazipuuza.

  • 82. Nao walikuwa wakichonga majumba katika milima kwa amani.

  • 83. Basi ukelele ukawatwaa asubuhi.

  • 84. Hayakuwafaa waliyo kuwa wakiyachuma.

  • 85. Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ila kwa ajili ya Haki. Na hakika Kiyama kitafika. Basi samehe msamaha mzuri.

  • 86. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Muumbaji Mjuzi.

  • 87. Na tumekupa Aya saba zinazo somwa mara kwa mara, na Qur`ani Tukufu.

  • 88. Usivitumbulie macho yako vitu tulivyo waneemesha makundi fulani kati yao, wala usiwahuzunikie. Na wainamishie bawa lako (la huruma) Waumini.

  • 89. Na sema: Hakika mimi ni mwonyaji mwenye kubainisha.

  • 90. Kama hivyo tuliwateremshia walio gawa,

  • 91. Ambao wakaifanya Qur`ani vipande vipande.

  • 92. Basi Naapa kwa Mola wako Mlezi! Tutawahoji wote,

  • 93. Kwa waliyo kuwa wakiyatenda.

  • 94. Basi wewe yatangaze uliyo amrishwa, na jitenge na washirikina.

  • 95. Hakika Sisi tunatosha kukukinga na wanao kejeli.

  • 96. Hao wanao fanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu yupo mungu mwingine. Basi, watakuja jua!

  • 97. Na Sisi tunajua kwa hakika kuwa wewe kifua chako kinaona dhiki kwa hayo wayasemayo.

  • 98. Basi mtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi, na uwe miongoni wanao msujudia.

  • 99. Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie Yakini.