• 1. T`aa Siin Miim. (T`. S. M.)

  • 2. Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha.

  • 3. Huenda labda ukajikera nafsi yako kwa kuwa hawawi Waumini.

  • 4. Tunge penda tungeli wateremshia kutoka mbinguni Ishara zikanyenyekea shingo zao.

  • 5. Wala hauwafikii ukumbusho mpya kutoka kwa Arrahman ila wao hujitenga nao.

  • 6. Kwa yakini wamekanusha; kwa hivyo zitakuja wafikia khabari za yale waliyo kuwa wakiyafanyia mzaha.

  • 7. Je! Hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri?

  • 8. Hakika katika haya zipo Ishara. Lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

  • 9. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

  • 10. Na Mola wako Mlezi, alipo mwita Musa, akamwambia: Fika kwa watu madhaalimu,

  • 11. Watu wa Firauni. Hawaogopi?

  • 12. Akasema: Hakika mimi nachelea wasinikanushe.

  • 13. Na kifua changu kina dhiki, na ulimi wangu haukunjuki vyema. Basi mtumie ujumbe Harun.

  • 14. Na wao wana kisasi juu yangu, kwa hivyo naogopa wasije kuniuwa.

  • 15. Akasema: Siyo hivyo kabisa! Nendeni na miujiza yetu. Hakika Sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza.

  • 16. Basi mfikieni Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

  • 17. Waachilie Wana wa Israili wende nasi.

  • 18. (Firauni) akasema: Sisi hatukukulea wewe utotoni, na ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi?

  • 19. Na ukatenda kitendo chako ulicho tenda, nawe ukawa miongoni mwa wasio na shukrani?

  • 20. (Musa) akasema: Nilitenda hayo hapo nilipo kuwa miongoni mwa wale walio potea.

  • 21. Basi nikakukimbieni nilipo kuogopeni, tena Mola wangu Mlezi akanitunukia hukumu, na akanijaalia niwe miongoni mwa Mitume.

  • 22. Na hiyo ndiyo neema ya kunisumbulia, na wewe umewatia utumwani Wana wa Israili?

  • 23. Firauni akasema: Na nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote?

  • 24. Akasema: Ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi ni wenye yakini.

  • 25. (Firauni) akawaambia walio mzunguka: Hamsikilizi?

  • 26. (Musa) akasema: Ndiye Mola wenu Mlezi, na Mola Mlezi wa baba zenu wa kwanza.

  • 27. (Firauni) akasema: Hakika huyu Mtume wenu aliye tumwa kwenu ni mwendawazimu.

  • 28. (Musa) akasema: Ndiye Mola Mlezi wa Mashariki na Magharibi na viliomo baina yao, ikiwa nyinyi mnatia akilini.

  • 29. (Firauni) akasema: Ukimfuata mungu mwengine asiye kuwa mimi, basi bila ya shaka nitakufunga gerezani.

  • 30. Akasema: Je! Ijapo kuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi?

  • 31. Akasema: Kilete basi, kama wewe ni katika wasemao kweli.

  • 32. Basi akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka wa kuonekana dhaahiri.

  • 33. Na akautoa mkono wake, na mara ukawa mweupe kwa watazamao.

  • 34. (Firauni) akawaambia waheshimiwa walio mzunguka: Hakika huyu ni mchawi mtaalamu.

  • 35. Anataka kukutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake. Basi mna shauri gani?

  • 36. Wakasema: Mpe muda yeye na nduguye na uwatume mijini wapigao mbiu ya mgambo.

  • 37. Wakuletee kila mchawi bingwa mtaalamu.

  • 38. Basi wakakusanywa wachawi wakati na siku maalumu.

  • 39. Na watu wakaambiwa: Je! Mtakusanyika?

  • 40. Huenda tutawafuata wachawi wakiwa wao ndio watakao shinda.

  • 41. Basi walipo kuja wachawi wakamwambia Firauni: Je! Tutapata ujira tukiwa sisi ndio tulio shinda?

  • 42. Naam! Na hakika mtakuwa katika watu wa mbele.

  • 43. Musa akwaambia: Tupeni mnavyo taka kutupa.

  • 44. Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu za Firauni hakika sisi hapana shaka ni wenye kushinda.

  • 45. Musa tena akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza walivyo vizua.

  • 46. Hapo wachawi walipinduka wakasujudu.

  • 47. Wakasema: Tunamuamini Mola Mlezi wa walimwengu wote.

  • 48. Mola Mlezi wa Musa na Harun.

  • 49. (Firauni) akasema: Je! Mmemuamini kabla sijakuruhusuni? Bila ya shaka yeye basi ndiye mkubwa wenu aliye kufunzeni uchawi. Basi mtakuja jua! Nitakata mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakubandikeni misalabani nyote.

  • 50. Wakasema: Haidhuru, kwani sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi.

  • 51. Hakika sisi tunatumai Mola wetu Mlezi atatusamehe makosa yetu, kwa kuwa ndio wa kwanza wa kuamini.

  • 52. Na tulimuamrisha Musa kwa wahyi: Nenda na waja wangu wakati wa usiku. Kwa hakika mtafuatwa.

  • 53. Basi Firauni akawatuma mijini wapiga mbiu za mgambo.

  • 54. (Wakieneza): Hakika hawa ni kikundi kidogo.

  • 55. Nao wanatuudhi.

  • 56. Na sisi ni wengi, wenye kuchukua hadhari.

  • 57. Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem,

  • 58. Na makhazina, na vyeo vya hishima,

  • 59. Kadhaalika; na tukawarithisha hayo Wana wa Israili.

  • 60. Basi wakawafuata lilipo chomoza jua.

  • 61. Na yalipo onana majeshi mawili haya, watu wa Musa wakasema: Hakika sisi bila ya shaka tumepatikana!

  • 62. (Musa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa!

  • 63. Tulimletea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa.

  • 64. Na tukawajongeza hapo wale wengine.

  • 65. Tukawaokoa Musa na walio kuwa pamoja naye wote.

  • 66. Kisha tukawazamisha hao wengine.

  • 67. Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara; lakini wengi wao si katika wenye kuamini.

  • 68. Na kwa hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

  • 69. Na wasomee khabari za Ibrahim.

  • 70. Alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?

  • 71. Wakasema: Tunaabudu masanamu, daima tunayanyenyekea.

  • 72. Akasema: Je! Yanakusikieni mnapo yaita?

  • 73. Au yanakufaeni, au yanakudhuruni?

  • 74. Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo.

  • 75. Je! Mmewaona hawa mnao waabudu-

  • 76. Nyinyi na baba zenu wa zamani?

  • 77. Kwani hakika hao ni adui zangu, isipo kuwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

  • 78. Ambaye ndiye aliye niumba, na Yeye ndiye ananiongoa,

  • 79. Na ambaye ndiye ananilisha na kuninywesha.

  • 80. Na ninapo ugua ni Yeye ndiye anaye niponesha.

  • 81. Na ambaye atanifisha, na kisha atanihuisha.

  • 82. Na ambaye ndiye ninaye mtumai kunisamehe makosa yangu Siku ya Malipo.

  • 83. Mola wangu Mlezi! Nitunukie hukumu na uniunganishe na watendao mema.

  • 84. Na unijaalie nitajwe kwa wema na watu watakao kuja baadaye.

  • 85. Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema.

  • 86. Na umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu.

  • 87. Wala usinihizi Siku watapo fufuliwa.

  • 88. Siku ambayo kwamba mali hayato faa kitu wala wana.

  • 89. Isipo kuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi.

  • 90. Na Pepo itasogezwa kwa wachamngu.

  • 91. Na Jahannamu itadhihirishwa kwa wapotovu.

  • 92. Na wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwaabudu

  • 93. Badala ya Mwenyezi Mungu? Je! Wanakusaidieni, au wanajisaidia wenyewe?

  • 94. Basi watavurumizwa humo wao na hao wakosefu,

  • 95. Na majeshi ya Ibilisi yote.

  • 96. Watasema, na hali ya kuwa wanazozana humo:

  • 97. Wallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio dhaahiri,

  • 98. Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote.

  • 99. Na hawakutupoteza ila wale wakosefu.

  • 100. Basi hatuna waombezi.

  • 101. Wala rafiki wa dhati.

  • 102. Laiti tungeli pata kurejea tena tungeli kuwa katika Waumini.

  • 103. Hakika katika haya ipo Ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

  • 104. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

  • 105. Kaumu ya Nuhu waliwakadhibisha Mitume.

  • 106. Alipo waambia ndugu yao, Nuhu: Je! Hamchimngu?

  • 107. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.

  • 108. Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit`iini mimi.

  • 109. Na sikutakini juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

  • 110. Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit`iini mimi.

  • 111. Wakasema: Je! Tukuamini wewe, hali wanao kufuata ni watu wa chini?

  • 112. Akasema: Nayajuaje waliyo kuwa wakiyafanya?

  • 113. Hisabu yao haiko ila kwa Mola wao Mlezi, laiti mngeli tambua!

  • 114. Wala mimi si wa kuwafukuza Waumini.

  • 115. Mimi si cho chote ila ni Mwonyaji wa dhaahiri shaahiri.

  • 116. Wakasema: Ikiwa huachi, ewe Nuhu, bila ya shaka utapigwa mawe.

  • 117. Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikanusha.

  • 118. Basi hukumu baina yangu na wao kwa hukumu yako, na uniokoe mimi na walio pamoja nami, Waumini.

  • 119. Kwa hivyo tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye katika marikebu iliyo sheheni.

  • 120. Kisha tukawazamisha baadaye walio bakia.

  • 121. Hakika katika haya ipo Ishara, lakini si wengi wao walio kuwa Waumini.

  • 122. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

  • 123. Kina A`d waliwakanusha Mitume.

  • 124. Alipo waambia ndugu yao, Hud: Je! Hamchimngu?

  • 125. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.

  • 126. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit`iini mimi.

  • 127. Wala sikutakeni juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

  • 128. Je! Mnajenga juu ya kila mnyanyuko kumbusho la kufanyia upuuzi?

  • 129. Na mnajenga majengo ya fakhari kama kwamba mtaishi milele!

  • 130. Na mnapo tumia nguvu mnatumia nguvu kwa ujabari.

  • 131. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit`iini.

  • 132. Na mcheni aliye kupeni haya mnayo yajua.

  • 133. Amekupeni wanyama wa kufuga na wana.

  • 134. Na mabustani na chemchem.

  • 135. Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Kubwa.

  • 136. Wakasema: Ni mamoja kwetu, ukitupa mawaidha au hukuwa miongoni mwa watoao mawaidha.

  • 137. Haya si chochote ila ni mtindo wa watu wa tokea zamani.

  • 138. Wala sisi hatutaadhibiwa.

  • 139. Wakamkanusha; nasi tukawaangamiza. Hakika bila ya shaka katika haya ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.

  • 140. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

  • 141. Kina Thamud waliwakanusha Mitume.

  • 142. Alipo waambia ndugu yao Saleh: Je! Hamumchimngu?

  • 143. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.

  • 144. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit`iini.

  • 145. Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

  • 146. Je! Mtaachwa salama usalimina katika haya yaliyopo hapa?

  • 147. Katika mabustani, na chemchem?

  • 148. Na konde na mitende yenye makole yaliyo wiva.

  • 149. Na mnachonga milimani majumba kwa ustadi.

  • 150. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit`iini mimi.

  • 151. Wala msit`ii amri za walio pindukia mipaka,

  • 152. Ambao wanafanya ufisadi katika nchi, wala hawatengenezi.

  • 153. Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa walio rogwa.

  • 154. Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi. Basi lete Ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.

  • 155. Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalumu.

  • 156. Wala msimguse kwa uwovu, isije ikakushikeni adhabu ya Siku Kubwa.

  • 157. Lakini wakamuuwa, na wakawa wenye kujuta.

  • 158. Basi ikawapata adhabu. Hakika katika hayo ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.

  • 159. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

  • 160. Watu wa Lut`i waliwakanusha Mitume.

  • 161. Alipo waambia ndugu yao, Lut`i: Je! Hamumchimngu?

  • 162. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu kwenu.

  • 163. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nit`iini mimi.

  • 164. Wala mimi sikutakini ujira juu yake; ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

  • 165. Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume?

  • 166. Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnao ruka mipaka!

  • 167. Wakasema: Ewe Lut`i! Usipo acha, hapana shaka utakuwa miongoni mwa wanao tolewa mji!

  • 168. Akasema: Hakika mimi ni katika wanao kichukia hichi kitendo chenu.

  • 169. Mola wangu Mlezi! Niokoe mimi na ahali zangu na haya wayatendayo.

  • 170. Basi tukamwokoa yeye na ahali zake wote,

  • 171. Isipo kuwa kikongwe katika walio kaa nyuma.

  • 172. Kisha tukawaangamiza wale wengine.

  • 173. Na tukawanyeshea mvua, basi ni ovu mno mvua ya waliyo onywa.

  • 174. Hakika katika hayo ipo Ishara. Na hawakuwa wengi wao wenye kuamini.

  • 175. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

  • 176. Watu wa Machakani waliwakanusha Mitume.

  • 177. Shuaibu alipo waambia: Je! Hamfanyi mkamchamngu?

  • 178. Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.

  • 179. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nit`iini mimi.

  • 180. Wala sikutakini ujira juu yake. Ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

  • 181. Timizeni kipimo sawa sawa, wala msiwe katika wanao punja.

  • 182. Na pimeni kwa haki iliyo nyooka;

  • 183. Wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye jeuri kwa ufisadi.

  • 184. Na mcheni aliye kuumbeni nyinyi na vizazi vilivyo tangulia.

  • 185. Wakasema: Hakika wewe ni katika walio rogwa.

  • 186. Na wewe si chochote ila ni mtu tu kama sisi, na kwa yakini tunakuona wewe ni katika waongo.

  • 187. Hebu tuangushie vipande kutoka mbinguni ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.

  • 188. Akasema: Mola wangu Mlezi anajua zaidi mnayo yatenda.

  • 189. Basi walimkanusha, na ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa.

  • 190. Hakika katika hayo ipo Ishara, lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.

  • 191. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

  • 192. Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

  • 193. Ameuteremsha Roho muaminifu,

  • 194. Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji,

  • 195. Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi.

  • 196. Na hakika bila ya shaka haya yamo katika Vitabu vya kale.

  • 197. Je! Haikuwa kwao ni Ishara kwamba wanayajua haya wanazuoni wa Wana wa Israili?

  • 198. Na lau kuwa tungeli iteremsha juu ya mmoja wa wasio kuwa Waarabu,

  • 199. Na akawasomea, wasingeli kuwa wenye kuamini.

  • 200. Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za wakosefu.

  • 201. Hawataiamini mpaka waione adhabu chungu.

  • 202. Basi itawafikia kwa ghafla, na hali hawana khabari.

  • 203. Na watasema: Je, tutapewa muhula?

  • 204. Basi, je, wanaihimiza adhabu yetu?

  • 205. Waonaje kama tukiwastarehesha kwa miaka,

  • 206. Kisha yakawafikia waliyo kuwa wakiahidiwa,

  • 207. Yatawafaa nini yale waliyo stareheshewa?

  • 208. Wala hatukuangamiza mji wo wote ila ulikuwa na waonyaji -

  • 209. Kuwa ni ukumbusho. Wala Sisi hatukuwa wenye kudhulumu.

  • 210. Wala Mashet`ani hawakuteremka nayo,

  • 211. Wala haitakiwi kwao, na wala hawawezi.

  • 212. Hakika hao wametengwa na kusikia.

  • 213. Basi usimwombe mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakao adhibiwa.

  • 214. Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe.

  • 215. Na watwae kwa upole wanao kufuata miongoni mwa Waumini.

  • 216. Na ikiwa watakuasi basi sema: Mimi najitenga mbali na hayo mnayo yatenda.

  • 217. Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.

  • 218. Ambaye anakuona unapo simama,

  • 219. Na mageuko yako kati ya wanao sujudu.

  • 220. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua.

  • 221. Je! Nikwambieni nani wanawashukia Mashet`ani?

  • 222. Wanamshukia kila mzushi mkubwa mwingi wa dhambi.

  • 223. Wanawapelekea yale wanayo yasikia; na wengi wao ni waongo.

  • 224. Na watungaji mashairi ni wapotofu ndio wanawafuata.

  • 225. Je! Huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde?

  • 226. Na kwamba wao husema wasiyo yatenda?

  • 227. Isipo kuwa wale walio amini, na wakatenda mema, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wakajitetea wanapo dhulumiwa. Na wanao dhulumu watakuja jua mgeuko gani watakao geuka.