• 1. Qaaf. Naapa kwa Qur`ani tukufu!

  • 2. Bali wanastaajabu kwamba amewafikia mwonyaji kutoka miongoni mwao, na wakasema makafiri: Hili ni jambo la ajabu!

  • 3. Ati tukifa na tukawa udongo...? Kurejea huko kuko mbali!

  • 4. Hakika Sisi tunajua kiasi cha kila kinacho punguzwa na ardhi kutokana nao. Na kwetu kipo Kitabu kinacho hifadhi yote.

  • 5. Lakini waliikanusha Haki ilipo wajia; kwa hivyo wamo katika mambo ya mkorogo.

  • 6. Je! Hawaangalii mbingu zilizo juu yao! Vipi tulivyo zijenga, na tukazipamba. Wala hazina nyufa.

  • 7. Na ardhi tumeitandaza na tukaiwekea milima, na tukaiotesha mimea mizuri ya kila namna.

  • 8. Yawe haya ni kifumbua macho na ukumbusho kwa kila mja mwenye kuelekea.

  • 9. Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji yaliyo barikiwa, na kwa hayo tukaotesha mabustani na nafaka za kuvunwa.

  • 10. Na mitende mirefu yenye makole yaliyo zaa kwa wingi,

  • 11. Ili iwe ni riziki kwa waja wangu. Na tukaifufua kwa maji nchi iliyo kuwa imekufa. Kama hivyo ndivyo utakavyo kuwa ufufuaji.

  • 12. Kabla yao walikadhibisha kaumu ya Nuhu na wakaazi wa Rassi na Thamudi.

  • 13. Na A`di na Firauni na kaumu ya Lut`i.

  • 14. Na wakaazi wa Machakani, na watu wa Tubbaa`. Wote hao waliwakanusha Mitume, kwa hivyo onyo likathibitika juu yao.

  • 15. Kwani tulichoka kwa kuumba mara ya kwanza. Bali wao wamo katika shaka tu juu ya umbo jipya.

  • 16. Na hakika tumemuumba mtu, nasi tunayajua yanayo mpitikia katika nafsi yake. Na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingoni mwake.

  • 17. Wanapo pokea wapokeaji wawili, wanao kaa kuliani na kushotoni.

  • 18. Hatamki neno ila karibu yake yupo mwangalizi tayari.

  • 19. Na uchungu wa kutoka roho utamjia kwa haki. Hayo ndiyo uliyo kuwa ukiyakimbia.

  • 20. Na litapulizwa baragumu. Hiyo ndiyo Siku ya Miadi.

  • 21. Na kila nafsi itakuja na pamoja nayo mchungaji na shahidi.

  • 22. (Aambiwe): Kwa hakika ulikuwa umeghafilika na haya; basi leo tumekuondolea pazia lako, na kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali.

  • 23. Na mwenzake atasema: Huyu niliye naye mimi kesha tayarishwa.

  • 24. Mtupeni katika Jahannamu kila kafiri mwenye inda,

  • 25. Akatazaye kheri, arukaye mipaka, mwenye kutia shaka,

  • 26. Aliye weka mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Basi mtupeni katika adhabu kali.

  • 27. Mwenzake aseme: Ee Mola wetu Mlezi! Sikumpoteza mimi, bali yeye mwenyewe alikuwa katika upotovu wa mbali.

  • 28. (Mwenyezi Mungu) aseme: Msigombane mbele yangu. Nilikuleteeni mbele onyo langu.

  • 29. Mbele yangu haibadilishwi kauli, wala Mimi siwadhulumu waja wangu.

  • 30. Siku tutapo iambia Jahannamu: Je! Umejaa? Nayo itasema: Je! Kuna ziada?

  • 31. Na Pepo italetwa karibu kwa ajili ya wachamngu, haitakuwa mbali.

  • 32. Haya ndiyo mnayo ahidiwa kwa kila mwenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu na akajilinda.

  • 33. Mwenye kumwogopa Mwingi wa Rehema hali kuwa hamwoni, na akaja kwa moyo ulio elekea-

  • 34. (Ataambiwa) ingieni kwa salama. Hiyo ndiyo siku ya daima dawamu.

  • 35. Humo watapata wakitakacho, na kwetu yako ya ziada.

  • 36. Na kaumu ngapi tuliziangamiza kabla yao walio kuwa na nguvu zaidi kuliko hawa! Nao walitanga tanga katika nchi nyingi. Je! Walipata pa kukimbilia?

  • 37. Hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au akatega sikio naye yupo anashuhudia.

  • 38. Na bila ya shaka Sisi tumeziumba mbingu na ardhi na vilio baina yao mnamo siku sita; na wala hayakutugusa machofu.

  • 39. Basi vumilia kwa hayo wasemayo, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa.

  • 40. Na katika usiku pia mtakase, na baada ya kusujudu.

  • 41. Na sikiliza siku atapo nadi mwenye kunadi kutoka pahala karibu.

  • 42. Siku watakapo sikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku ya kufufuka.

  • 43. Hakika Sisi tunahuisha na tunafisha, na kwetu Sisi ndio marejeo.

  • 44. Siku itapo wapasukia ardhi mbio mbio! Mkusanyo huo kwetu ni mwepesi.

  • 45. Sisi tunajua kabisa wayasemayo. Wala wewe si mwenye kuwatawalia kwa ujabari. Basi mkumbushe kwa Qur`ani anaye liogopa onyo.