27. An-Naml - Qurani
- 1. T`aa Siin. (T`. S.), Hizi ni Aya za Qur`ani na Kitabu kinacho bainisha;
- 2. Uwongofu na bishara kwa Waumini,
- 3. Ambao wanashika Sala, na wanatoa Zaka, na Akhera wana yakini nayo.
- 4. Kwa hakika wale wasio iamini Akhera tumewapambia vitendo vyao, kwa hivyo wanatangatanga ovyo.
- 5. Hao ndio watapata adhabu mbaya kabisa, na hao katika Akhera ndio watapata khasara zaidi.
- 6. Na hakika wewe unafundishwa Qur`ani inayo tokana kwake Mwenye hikima Mwenye kujua.
- 7. (Kumbuka) Musa alipo waambia ahali zake: Hakika nimeona moto, nitakwenda nikuleteeni khabari, au nitakuleteeni kijinga kinacho waka ili mpate kuota moto.
- 8. Basi alipo fika ilinadiwa: Amebarikiwa aliomo katika moto huu na walioko pembezoni mwake. Na ametakasika Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.