• 1. Naapa kwa alfajiri,

  • 2. Na kwa masiku kumi,

  • 3. Na kwa viwili viwili na kimoja kimoja,

  • 4. Na kwa usiku unapo pita,

  • 5. Je! Hapana katika haya kiapo kwa mwenye akili?

  • 6. Kwani hukuona jinsi Mola wako Mlezi alivyo wafanya kina A`di?

  • 7. Wa Iram, wenye majumba marefu?

  • 8. Ambao haukuumbwa mfano wake katika nchi?

  • 9. Na Thamudi walio chonga majabali huko bondeni?

  • 10. Na Firauni mwenye vigingi?

  • 11. Ambao walifanya jeuri katika nchi?

  • 12. Wakakithirisha humo ufisadi?

  • 13. Basi Mola wako Mlezi aliwapiga mjeledi wa adhabu.

  • 14. Hakika Mola wako Mlezi yupo kwenye mavizio anawavizia.

  • 15. Ama mtu anapo jaribiwa na Mola wake Mlezi, akamkirimu na akamneemesha, husema: Mola wangu Mlezi amenikirimu!

  • 16. Na ama anapo mjaribu akampunguzia riziki yake, husema: Mola wangu Mlezi amenitia unyonge!

  • 17. Sivyo hivyo! Bali nyinyi hamuwakirimu mayatima,

  • 18. Wala hamhimizani kulisha masikini;

  • 19. Na mnakula urithi kwa ulaji wa pupa,

  • 20. Na mnapenda mali pendo la kupita kiasi.

  • 21. Sivyo hivyo! Itakapo vunjwa ardhi vipande vipande,

  • 22. Na akaja Mola wako Mlezi na Malaika safu safu,

  • 23. Na ikaletwa Jahannamu siku hiyo, siku hiyo mtu atakumbuka! Lakini kukumbuka huko kutamfaa nini?

  • 24. Atasema: Laiti ningeli jitangulizia kwa uhai wangu!

  • 25. Basi siku hiyo hataadhibu yeyote namna ya kuadhibu kwake.

  • 26. Wala hatafunga yeyote kama kufunga kwake.

  • 27. Ewe nafsi iliyo tua!

  • 28. Rejea kwa Mola wako Mlezi umeridhika, na umemridhisha.

  • 29. Basi ingia miongoni mwa waja wangu,

  • 30. Na ingia katika Pepo yangu.