• 1. Litakapo tukia hilo Tukio

  • 2. Hapana cha kukanusha kutukia kwake.

  • 3. Literemshalo linyanyualo,

  • 4. Itakapo tikiswa ardhi kwa mtikiso,

  • 5. Na milima itapo sagwasagwa,

  • 6. Iwe mavumbi yanayo peperushwa,

  • 7. Na nyinyi mtakuwa namna tatu:-

  • 8. Basi watakuwepo wa kuliani; je, ni wepi wa kuliani?

  • 9. Na wa kushotoni; je, ni wepi wa kushotoni?

  • 10. Na wa mbele watakuwa mbele.

  • 11. Hao ndio watakao karibishwa

  • 12. Katika Bustani zenye neema.

  • 13. Fungu kubwa katika wa mwanzo,

  • 14. Na wachache katika wa mwisho.

  • 15. Watakuwa juu ya viti vya fakhari vilivyo tonewa.

  • 16. Wakiviegemea wakielekeana.

  • 17. Wakitumikiwa na wavulana wa ujana wa milele,

  • 18. Kwa vikombe na mabirika na bilauri za vinywaji kutoka chemchem safi.

  • 19. Hawataumwa kichwa kwa vinywaji hivyo wala hawatoleweshwa.

  • 20. Na matunda wayapendayo,

  • 21. Na nyama za ndege kama wanavyo tamani.

  • 22. Na Mahurulaini,

  • 23. Walio kama mfano wa lulu zilio hifadhiwa.

  • 24. Ni malipo kwa waliyo kuwa wakiyatenda.

  • 25. Humo hawatasikia porojo wala maneno ya dhambi,

  • 26. Isipo kuwa maneno ya Salama, Salama.

  • 27. Na wale wa mkono wa kulia, ni yepi yatakuwa ya wa kuliani?

  • 28. Katika mikunazi isiyo na miba,

  • 29. Na migomba iliyo pangiliwa,

  • 30. Na kivuli kilicho tanda,

  • 31. Na maji yanayo miminika,

  • 32. Na matunda mengi,

  • 33. Hayatindikii wala hayakatazwi,

  • 34. Na matandiko yaliyo nyanyuliwa.

  • 35. Hakika Sisi tutawaumba (Mahurulaini) upya,

  • 36. Na tutawafanya vijana,

  • 37. Wanapendana na waume zao, hirimu moja.

  • 38. Kwa ajili ya watu wa kuliani.

  • 39. Fungu kubwa katika wa mwanzo,

  • 40. Na fungu kubwa katika wa mwisho.

  • 41. Na watu wa kushotoni; je ni yepi ya wa kushotoni?

  • 42. Katika upepo wa moto, na maji yanayo chemka,

  • 43. Na kivuli cha moshi mweusi,

  • 44. Si cha kuburudisha wala kustarehesha.

  • 45. Hakika hao walikuwa kabla ya haya wakiishi maisha ya anasa.

  • 46. Na walikuwa wakishikilia kufanya madhambi makubwa,

  • 47. Na walikuwa wakisema: Tutakapo kufa na tukawa udongo na mafupa, ati ndio tutafufuliwa?

  • 48. Au baba zetu wa zamani?

  • 49. Sema: Hakika wa zamani na wa mwisho

  • 50. Bila ya shaka watakusanywa kwa wakati wa siku maalumu.

  • 51. Kisha nyinyi, mlio potea, mnao kanusha,

  • 52. Kwa yakini mtakula mti wa Zaqqumu.

  • 53. Na kwa mti huo mtajaza matumbo.

  • 54. Na juu yake mtakunywa maji yanayo chemka.

  • 55. Tena mtakunywa kama wanavyo kunywa ngamia wenye kiu.

  • 56. Hiyo ndiyo karamu yao Siku ya Malipo.

  • 57. Sisi tumekuumbeni; basi hamsadiki?

  • 58. Je! Mnaiona mbegu ya uzazi mnayo idondokeza?

  • 59. Je! Mnaiumba nyinyi, au ni Sisi ndio Waumbaji?

  • 60. Sisi tumekuwekeeni mauti; na wala Sisi hatushindwi

  • 61. Kuwaleta wengine badala yenu na kukuumbeni nyinyi kwa umbo msilo lijua.

  • 62. Na bila ya shaka mlikwisha jua umbo la kwanza, basi kwa nini hamkumbuki?

  • 63. Je! Mnaona makulima mnayo yapanda?

  • 64. Je! Ni nyinyi mnayo yaotesha au ni Sisi ndio wenye kuotesha?

  • 65. Tungeli taka tungeli yafanya yakawa mapepe, mkabaki mnastaajabu,

  • 66. Mkisema: Hakika sisi tumegharimika;

  • 67. Bali sisi tumenyimwa.

  • 68. Je! Mnayaona maji mnayo yanywa?

  • 69. Je! Ni nyinyi mnayo yateremsha kutoka mawinguni au ni Sisi ndio wenye kuyateremsha?

  • 70. Tungeli penda tungeli yafanya ya chumvi. Basi mbona hamshukuru?

  • 71. Je! Mnauona moto mnao uwasha?

  • 72. Ni nyinyi mlio uumba mti wake au Sisi ndio Waumbaji?

  • 73. Sisi tumeufanya uwe ni ukumbusho na manufaa kwa walioko nyikani.

  • 74. Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkuu.

  • 75. Basi naapa kwa maanguko ya nyota,

  • 76. Na hakika bila ya shaka hichi ni kiapo kikubwa, laiti mngeli jua!

  • 77. Hakika hii bila ya shaka ni Qur`ani Tukufu,

  • 78. Katika Kitabu kilicho hifadhiwa.

  • 79. Hapana akigusaye ila walio takaswa.

  • 80. Ni uteremsho unao toka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

  • 81. Ni maneno haya ndiyo nyinyi mnayapuuza?

  • 82. Na badala ya kushukuru kwa riziki yenu mnafanya kuwa mnakadhibisha?

  • 83. Yawaje basi itakapo fika roho kwenye koo,

  • 84. Na nyinyi wakati huo mnatazama!

  • 85. Na Sisi tuko karibu zaidi naye kuliko nyinyi.

  • 86. Na lau kuwa nyinyi hamumo katika mamlaka yangu,

  • 87. Kwanini hamuirudishi hiyo roho, ikiwa nyinyi mnasema kweli?

  • 88. Basi akiwa miongoni mwa walio karibishwa,

  • 89. Basi ni raha, na manukato, na Bustani zenye neema.

  • 90. Na akiwa katika watu wa upande wa kulia,

  • 91. Basi ni Salamu kwako uliye miongoni mwa watu wa upande wa kulia.

  • 92. Na ama akiwa katika walio kadhibisha wapotovu,

  • 93. Basi karamu yake ni maji yanayo chemka,

  • 94. Na kutiwa Motoni.

  • 95. Hakika hii ndiyo haki yenye yakini.

  • 96. Basi litakase jina la Mola wako Mlezi aliye Mkubwa.