logo HARUN YAHYA

At-Takwir - QURAN - Harun Yahya

  • 1. Jua litakapo kunjwa,
  • 2. Na nyota zikazimwa,
  • 3. Na milima ikaondolewa,
  • 4. Na ngamia wenye mimba pevu watakapo achwa wasishughulikiwe,
  • 5. Na wanyama wa mwituni wakakusanywa,
  • 6. Na bahari zikawaka moto,
  • 7. Na nafsi zikaunganishwa,
  • 8. Na msichana aliye zikwa hai atapo ulizwa,
  • 9. Kwa kosa gani aliuliwa?
  • 10. Na madaftari yatakapo enezwa,
  • 11. Na mbingu itapo tanduliwa,
  • 12. Na Jahannamu itapo chochewa,
  • 13. Na Pepo ikasogezwa,
  • 14. Kila nafsi itajua ilicho kihudhurisha.
  • 15. Naapa kwa nyota zinapo rejea nyuma,
  • 16. Zinazo kwenda, kisha zikajificha,
  • 17. Na kwa usiku unapo pungua,
  • 18. Na kwa asubuhi inapo pambazuka,
  • 19. Kwamba hakika bila ya shaka hii ni kauli ya Mjumbe mtukufu,
  • 20. Mwenye nguvu na mwenye cheo kwa huyo Mwenye Kiti cha Enzi,
  • 21. Anaye t`iiwa, tena muaminifu.
  • 22. Na wala huyu mwenzenu hana wazimu.
  • 23. Na hakika yeye alimwona kwenye upeo wa macho ulio safi.
  • 24. Wala yeye si bakhili kwa mambo ya ghaibu.
  • 25. Wala hii si kauli ya Shetani maluuni.
  • 26. Basi mnakwenda wapi?
  • 27. Haikuwa hii ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote.
  • 28. Kwa yule miongoni mwenu anaye taka kwenda sawa.
  • 29. Wala nyinyi hamtataka isipo kuwa atake Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote.
SHIRIKI
Facebook
X
WhatsApp
Telegram
QR Code
QR Code