logo HARUN YAHYA

Al-Haqqah - QURAN - Harun Yahya

  • 1. Tukio la haki.
  • 2. Nini hilo Tukio la haki?
  • 3. Na nini kitakujuulisha nini hilo Tukio la haki?
  • 4. Thamudi na A`di waliukadhibisha Msiba unao situsha.
  • 5. Basi Thamudi waliangamizwa kwa balaa kubwa mno.
  • 6. Na ama A`di waliangamizwa kwa upepo mkali usio zuilika.
  • 7. Alio wapelekea masiku saba, na siku nane, mfululizo bila ya kusita. Utaona watu wamepinduka kama kwamba ni magongo ya mitende yalio wazi ndani.
  • 8. Basi je! Unamwona mmoja wao aliye baki?
  • 9. Na Firauni na walio mtangulia, na miji iliyo pinduliwa chini juu, walileta khatia.
  • 10. Wakamuasi Mtume wa Mola wao Mlezi, ndipo Yeye Mola akawakamata kwa mkamato ulio zidi nguvu.
  • 11. Maji yalipo furika Sisi tulikupandisheni katika safina,
  • 12. Ili tuyafanye hayo kuwa ni waadhi kwenu na kila sikio linalo sikia liyahifadhi.
  • 13. Na litapo pulizwa barugumu mpulizo mmoja tu,
  • 14. Na ardhi na milima ikaondolewa, na ikavunjwa kwa mvunjo mmoja,
  • 15. Siku hiyo ndio Tukio litatukia.
  • 16. Na mbingu zitapasuka, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu kabisa.
  • 17. Na Malaika watakuwa pembezoni mwa mbingu; na wanane juu ya hawa watakuwa wamebeba Kiti cha Enzi cha Mola wako Mlezi.
  • 18. Siku hiyo mtahudhurishwa - haitafichika siri yoyote yenu.
  • 19. Basi ama atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: Haya someni kitabu changu!
  • 20. Hakika nalijua ya kuwa nitapokea hisabu yangu.
  • 21. Basi yeye atakuwa katika maisha ya kupendeza,
  • 22. Katika Bustani ya juu,
  • 23. Matunda yake yakaribu.
  • 24. Waambiwe: Kuleni na mnywe kwa furaha kwa sababu ya mlivyo tanguliza katika siku zilizo pita.
  • 25. Na ama atakaye pewa kitabu chake katika mkono wake wa kushoto, basi yeye atasema: Laiti nisingeli pewa kitabu changu!
  • 26. Wala nisingeli jua nini hisabu yangu.
  • 27. Laiti mauti ndiyo yangeli kuwa ya kunimaliza kabisa.
  • 28. Mali yangu hayakunifaa kitu.
  • 29. Madaraka yangu yamenipotea.
  • 30. (Pasemwe): Mshikeni! Mtieni pingu!
  • 31. Kisha mtupeni Motoni!
  • 32. Tena mtatizeni katika mnyororo wenye urefu wa dhiraa sabiini!
  • 33. Kwani huyo hakika alikuwa hamuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu,
  • 34. Wala hahimizi kulisha masikini.
  • 35. Basi leo hapa hana jamaa wa kumwonea uchungu,
  • 36. Wala hana chakula ila usaha wa watu wa Motoni.
  • 37. Chakula hicho hawakili ila wakosefu.
  • 38. Basi naapa kwa mnavyo viona,
  • 39. Na msivyo viona,
  • 40. Kwa hakika hii ni kauli iliyo letwa na Mjumbe mwenye hishima.
  • 41. Wala si kauli ya mtunga mashairi. Ni machache sana mnayo yaamini.
  • 42. Wala si kauli ya kuhani. Ni machache mnayo yakumbuka.
  • 43. Ni uteremsho utokao kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
  • 44. Na lau kama angeli tuzulia baadhi ya maneno tu,
  • 45. Bila ya shaka tungeli mshika kwa mkono wa kulia,
  • 46. Kisha kwa hakika tungeli mkata mshipa mkubwa wa moyo!
  • 47. Na hapana yeyote katika nyinyi ambaye angeli weza kutuzuia.
  • 48. Kwa hakika hii ni mawaidha kwa wachamngu.
  • 49. Na hakika Sisi bila ya shaka tunajua kwamba miongoni mwenu wapo wanao kadhibisha.
  • 50. Na hakika bila ya shaka itakuwa ni majuto kwa wanao kataa.
  • 51. Na hakika hii bila ya shaka ni haki ya yakini.
  • 52. Basi litakase jina la Mola wako Mlezi Mtukufu.
SHIRIKI
Facebook
X
WhatsApp
Telegram
QR Code
QR Code