logo HARUN YAHYA

Al-Buruj - QURAN - Harun Yahya

  • 1. Naapa kwa mbingu yenye Buruji!
  • 2. Na kwa siku iliyo ahidiwa!
  • 3. Na kwa shahidi na kinacho shuhudiwa!
  • 4. Wameangamizwa watu wa makhandaki
  • 5. Yenye moto wenye kuni nyingi,
  • 6. Walipo kuwa wamekaa hapo,
  • 7. Na wao ni mashahidi wa yale waliyo kuwa wakiwafanyia Waumini.
  • 8. Nao hawakuona baya lolote kwao ila kuwa wakimuamini Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Msifiwa,
  • 9. Ambaye anao ufalme wa mbingu na ardhi; na Mwenyezi Mungu ni shaahidi wa kila kitu.
  • 10. Hakika walio wafitini Waumini wanaume na Waumini wanawake, kisha hawakutubu, basi watapata adhabu ya Jahannamu na watapata adhabu ya kuungua.
  • 11. Hakika walio amini na wakatenda mema watapata Bustani zenye mito ipitayo kati yake. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
  • 12. Hakika kutesa kwa Mola wako Mlezi ni kukali.
  • 13. Yeye ndiye anaye anzisha na ndiye anaye rejeza tena,
  • 14. Naye ni Mwenye kusamehe, Mwenye mapenzi,
  • 15. Mwenye Kiti cha Enzi, Mtukufu,
  • 16. Atendaye ayatakayo.
  • 17. Je! Zimekuwasilia khabari za majeshi?
  • 18. Ya Firauni na Thamudi?
  • 19. Lakini walio kufuru wamo katika kukadhibisha.
  • 20. Na Mwenyezi Mungu nyuma yao amewazunguka.
  • 21. Bali hii ni Qur`ani tukufu
  • 22. Katika Ubao Ulio Hifadhiwa.
SHIRIKI
Facebook
X
WhatsApp
Telegram
QR Code
QR Code